ABDULLAH MWINYI ATOA MAPENDEKEZO YA NAMNA SERIKALI ITAKAVYOPATA TRILIONI 8-12 KWA MWAKA
Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Abdullah Mwinyi, ametoa mapendekezo mbalimbali ya kisera na kikodi ambayo amesema yanaweza kuifanya Serikali kuongeza mapato yake kwa zaidi ya shilingi trilioni 8 kwa mwaka ikiwa yatafanyiwa kazi ipasavyo.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni leo Jumanne Juni 16, 2026 Mhe. Mwinyi amesema, kuwa pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), bado Tanzania ina nafasi kubwa ya kuongeza mapato yake kwa kupanua wigo wa walipakodi.
Amesema uwiano wa mapato ya Serikali kwa Pato la Taifa (Revenue to GDP Ratio) kwa sasa ni asilimia 13.5, kiwango ambacho ni cha chini ikilinganishwa na wastani wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao ni asilimia 16.
βWataalamu wa uchumi wanatuambia ili tuwe na mfumo wenye ufanisi tunapaswa kufikia angalau asilimia 15, na ili uchumi wetu uwe endelevu na kukua kwa kasi zaidi tunapaswa kufikia asilimia 18,β alisema.
Mbunge huyo ameeleza kuwa changamoto siyo TRA kwani kwa miaka mitatu mfululizo imekuwa ikivuka malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa zaidi ya asilimia 103, bali tatizo kubwa lipo katika idadi ndogo ya walipakodi waliopo kwenye mfumo rasmi.
Kwa mujibu wa Mhe. Mwinyi, tafiti zinaonesha kuwa asilimia 45 ya shughuli za kiuchumi nchini bado zipo nje ya mfumo wa kodi huku biashara ndogo na za kati milioni 1.8 zikiwa hazijasajiliwa katika mfumo huo.
Amesema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakikwepa kuingia kwenye mfumo wa kodi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo viwango vya kodi kuwa vikubwa, ugumu wa utaratibu wa ulipaji kodi pamoja na hatua kali za utekelezaji zinazochukuliwa dhidi yao.
βTunapaswa kuwa na mfumo wa kodi unaozingatia tofauti kati ya biashara kubwa na biashara ndogo. Tukirahisisha mazingira kwa wafanyabiashara wadogo kuingia kwenye mfumo wa kodi, tutapanua wigo wa walipakodi na kuongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa,β alisema.
Mhe. Mwinyi amebainisha kuwa kuingiza biashara ndogo na za kati milioni 1.8 kwenye mfumo rasmi wa kodi kunaweza kuiwezesha Serikali kukusanya kati ya shilingi trilioni 8 hadi trilioni 12 za ziada kila mwaka, fedha ambazo zinaweza kuelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii.
Aidha, amependekeza kuondolewa kwa kodi inayotozwa kwenye retained profits yaani faida inayobaki ndani ya kampuni kwa ajili ya kuendeleza biashara na uwekezaji wa baadaye.
Amesema hapo awali kodi hiyo ilikuwa ikitozwa kwa kiwango cha asilimia 30 lakini katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 imepunguzwa hadi asilimia 15, hatua aliyoipongeza huku akisisitiza kuwa kuondolewa kabisa kwa kodi hiyo kutachochea uwekezaji zaidi, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa.