Umekua wakati mzuri leo kukutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Peter Nalitolela. Mazungumzo yetu yamejikita katika kuboresha mahusiano baina ya taasisi zetu ili kuweza kutoa mchango zaidi katika masoko ya mitaji na dhamana.
Sambamba na hilo tumeweza kushiriki katika fainali za Shindano la Utafiti chini ya uratibu wa CFA Society E.A(Chartered Financial Analysts Society East Africa). Shindano hili la kila mwaka linatoa fursa kwa wanafunzi wa vyuo kupata mafunzo ya vitendo katika uchambuzi wa masuala ya fedha ambapo kwa mwaka 2024/25 Benki ya CRDB imechaguliwa kuwa taasisi ambayo shindano hilo litajikita katika kufanyia utafiti.
Shindano la mwaka huu litahusisha wanafunzi wa vyuo kutoka Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda ambapo mbali na kudhamini shindano hilo, kwa niaba ya Benki yetu nimeahidi kutoa nafasi 5 kwa wanafunzi kutoka Tanzania watakaofanya vizuri kupata ajira. Nimshukuru kaka yangu, CPA Nicodemus Mkama kwa kuahidi kuwa CMSA itawapa mafunzo ya ziada ya vitendo wanafunzi hao watano kabla ya kuajiriwa na Benki yetu.