Kuna watu unawasiliana nao kwa karibu sana kwa vile mnafanya kazi pamoja na mnakutana mara kwa mara. Ukihama sehemu inayowakutanisha mnabaki kuwa ‘strangers.’ Wengine mnawasiliana kwa ukaribu sana maana kuna tatizo fulani linawaunganisha. Tatizo hilo likitatuliwa mnabaki watu mnaofahamiana msio na mengi ya kuzungumzia. Wengine mko karibu maana mnaamini kitu kinachofanana. Saa nyingine hata sio imani ni watu tu mnaochangia hofu na wasiwasi wa kisichofahamika. Ukiwa huru kidogo kwa mawazo ukaweza kutofautiana na mtazamo tofauti, unakuwa ‘stranger’ kwa watu wengi wa hivi.
Wakati mwingine, hata kile kinachoitwa mapenzi kina kinaenda kwa kanuni ile ile. Kinganishi ni shida za angalau mmoja wapo. Ukweli ni kwamba umasikini ni kiunganishi kikubwa cha mahusiano mengi. Huchaguliwi na mtu kwa vile unamfaa bali kwa uwezo wako kuzitafutia ufumbuzi shida zinazomsumbua mwenzako na familia yake. Ikitokea umekosa raslimali za kutatua shida zake unaanza kuonekana ‘toxic’ na huna mahusiano yenye ‘future’. Saa nyingine raslimali inaweza kuwa kitu chochote kinachofukia ombwe la mwenzio. Uko kwenye mahusiano kwa sababu mwenzako na kitu fulani kinachokupunguzia hofu, wasiwasi na kadhalika.
Unasema una maana gani Mshunuzi? Hoja ninayojaribu kuijenga hapa ni kutokulaumu sana watu wakipotea. Unapowalaumu watu kwa kuacha kuwasiliana na wewe pengine ni muhimu kukumbuka wengi unaofanya nazo kazi si marafiki; wengi unaofikiri ni marafiki ni watu mnaofahamiana, mnaokutana mara kwa mara, mnachangia hofu na huenda mna matatizo yanayofanana, mnasaidiana na, kwa hakika, kinachowaunganisha kikiondoka—kazi, ukaribu wa eneo, matatizo, connection, imani na kadhalika na mawasiliano yenu nayo yanakatika.
Ukiwa na mtu anayeendelea kuwa karibu na wewe hata mnapokuwa mbali, hamuonani mara kwa mara, hana anachonufaika na ukaribu wenu zaidi ya mawasiliano yanayodumisha uhusiano mshukuru Mungu. Ukiwa na mpenzi anayeweza kutenganisha shida zake, umasikini wake na mapenzi mshukuru Mungu. Heshimu mtu anayethamini uhusiano wenu, anayekutafuta kukusalimia hata kama hana tatizo linalohitaji ufumbuzi.