Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza kuwa Jumatano, tarehe 17 Juni 2026, itakuwa siku ya mapumziko kwa Zanzibar ili kuukaribisha Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448 Hijria.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa tamko hilo leo, tarehe 15 Juni 2026, Ikulu Zanzibar, ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa Serikali wa kuutambua Mwaka Mpya wa Kiislamu kuwa miongoni mwa siku muhimu Zanzibar.
Amesema siku hiyo itatoa fursa kwa Wananchi, hususan waumini wa dini ya Kiislamu, kuukarıbısha mwaka mpya kwa ibada, dua, na matendo mema, pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuijaalia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla amani, umoja na ustawi.
Alhaj Dkt. Mwinyi amewataka Wananchi kuutumia mwaka mpya huo kujitathmini, kuimarisha uchamungu, kusaidiana na kuendeleza maadili mema yanayojenga familia na Taifa lenye mshikamano.
Aidha, amezitaka taasisi za Serikali, taasisi binafsi, waajiri na Wananchi wote kuzingatia tangazo hilo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Rais Dkt. Mwinyi amewatakia Waislamu na wananchi wote heri ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1448 Hijria, akimuomba Mwenyezi Mungu aufanye kuwa mwaka wa kheri, amani, afya njema na maendeleo kwa wote.
#KitengeUpdates