Zaidi ya shilingi milioni 300 zimetumika kununua vifaa vya elimu na afya kwa shule za msingi wilaya za Bunda na Serengeti, mkoani Mara. Vifaa hivyo ni pamoja na madawati zaidi ya 3,000, vitanda, kompyuta, na vifaa vingine muhimu kwa shule, vyote vikitolewa na Shirika la Grumeti Reserves Limited kwa kushirikiana na Tawa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivi, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhifadhi Jamii alisema msaada huo ni sehemu ya jitihada za jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira, hususan katika mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti, kupitia mfuko wa uhifadhi wa SWICA.
Kwa wilaya ya Bunda, madawati 1,534 yamekabidhiwa, huku wilaya ya Serengeti ikipatiwa madawati 1,480. Vifaa vingine vinajumuisha vitanda 16, kompyuta 19, pamoja na miradi ya uwekeaji wa maji katika shule moja ya msingi. Aidha, vifaa vya Tehama vinapelekwa kwa shule zote zilizolengwa.
Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Angelina Marco, amepongeza jitihada za uhifadhi na kueleza kuwa matunda yake yanachangia maendeleo ya taifa.
Pia aliwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa wanyamapori. Vilevile, mkuu wa wilaya ya Bunda amewataka wananchi kuacha vitendo vya ujangili na kulinda mali ya taifa katika maeneo yao.