Mahakama ya Rufaa nchini Mauritania imetoa hukumu ya kifungo cha miaka 15 jela na faini ya dola milioni 3 kwa Rais wa zamani Mohamed Ould Abdel Aziz, baada ya kupinga hukumu ya awali ya kifungo cha miaka mitano iliyotolewa mwaka 2023.
Aziz, ambaye aliwahi kuongoza mapinduzi mawili nchini humo kabla ya kutawala kwa mihula miwili (2009–2019), alipatikana na hatia ya utakatishaji fedha na kujipatia utajiri kwa njia zisizo halali alipokuwa madarakani. Ripoti za uchunguzi zinaonesha kuwa alikusanya mali yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 70, hatua iliyosababisha yeye kuwekwa kizuizini tangu mwaka jana.
Kesi dhidi ya Aziz ni miongoni mwa matukio machache sana barani Afrika ambapo kiongozi wa juu wa zamani wa nchi amefikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa makosa ya kifisadi, jambo linaloibua maswali kuhusu uwajibikaji wa viongozi barani humo.
Licha ya hukumu hiyo, mawakili wa Aziz wanadai kesi hiyo ilichochewa kisiasa, wakisisitiza kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa uhalifu aliohusika nao.
Katika hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufaa iliyotolewa Jumatano, maafisa sita wakuu kutoka utawala wa Aziz waliondolewa mashtaka, mkwe wa Aziz alipatikana na hatia ya kosa la ushawishi na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.
Ingawa Mauritania ni nchi tajiri kwa rasilimali kama madini ya chuma, shaba, dhahabu, mafuta na gesi, bado inakabiliwa na kiwango kikubwa cha umaskini. Takribani asilimia 60 ya wananchi wanaishi katika hali duni, wengi wao wakitegemea kilimo cha kujikimu au vibarua visivyo rasmi, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.