Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza rasmi kuingia barabarani kupitia mikutano ya hadhara nchini kote, kikidai kuwa sauti za wapinzani zinaendelea kufinywa na vyombo vya dola huku serikali ikisusa kutenga fedha za Katiba Mpya kwenye bajeti kuu ya nchi.
βAkizungumza leo Juni 15, 2026 mbele ya Waandishi wa Habari, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia amesema ziara hizo zitaanza Ukanda wa Kusini, zikihusisha Kanda za Kusini, Nyasa na Magharibi kuanzia Juni 18 hadi Juni 26, 2026.
βRupia amekosoa bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 iliyotangazwa wiki iliyopita kwa kutotenga fungu lolote la mchakato wa Katiba, akionya kuwa ikifika mwaka 2028 utakuwa ni ucheleweshaji uliopitiliza.
β"Bado sauti zetu hazijasikika, bado sauti zetu zinafinywa na vyombo vya dola na CCM wanajimilikisha vyombo hivyo. Bajeti haina kipengele cha Katiba, na serikali haina mpango huo kwa mwaka huu wakati sisi tulishasema ikifika 2028 itakuwa ni 'too late' kuanza mchakato," amesema Brenda Rupia kwenye makao makuu ya chama hicho, Edwin House yaliyopo Mikocheni.
βKatika hatua nyingine, Rupia ameshtumu Jeshi la Polisi kwa kupora sare za chama hicho (kombati) na kofia kutoka kwa muuzaji mkuu, Ndugu Mjela, akidai kuwa kuna njama za kuwavalisha watu wao ili wafanye fujo na kuisingizia Chadema wakati wa operesheni hizo.
β
Ratiba ya mikutano hiyo itaanza Juni 18 huko Nachingwea, ikifuatiwa na Masasi (Juni 19), Songea Mjini (Juni 20), Njombe na Makambako (Juni 21), Mbarali (Juni 22), Mbeya Mjini (Juni 23), Tunduma (Juni 24), Mpanda (Juni 25) na kuhitimishwa Tabora Mjini mnamo Juni 26, 2026.