Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa kuna askari polisi amepigwa mkoani humo, likifafanua kuwa video inayozunguka imetengenezwa kwa nia ya uchonganishi.
Katika taarifa rasmi kwa umma iliyotolewa Jumapili, Juni 14, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejoa meeleza kuwa picha mjongeo (video) hiyo iliyowekwa mtandaoni na mwanaharakati Maria Sarungi haina ukweli wowote na haikutokea nchini Tanzania.
Uchunguzi wa kiufundi na kiintelijensia wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa matukio yanayoonekana katika video hiyo yalirekodiwa maeneo mengine nje ya nchi. Polisi wamedai kuwa picha hizo zilichukuliwa na kuunganishwa na maneno ya uongo ili kuaminisha umma kuwa tukio hilo limetokea jijini Arusha.
“Mkoani Arusha hakuna tukio lolote lililotokea kuhusiana na Askari kupigwa na inaonesha wazi kuwa picha mjongeo hiyo ilichukuliwa maeneo mengine nje ya nchi, kisha kutengenezewa maneno ya uongo”, imeeleza taarifa ya Kamanda wa Polisi.
Jeshi la Polisi limeeleza kusikitishwa na mwenendo wa baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuandaa maudhui yenye kupandikiza chuki kati ya vyombo vya dola na jamii. Kamanda amesisitiza kuwa vitendo hivyo ni vinyume cha makuzi, mila, desturi njema za Kitanzania, pamoja na mifumo ya kisheria inayosimamia mawasiliano ya kimtandao.
Polisi mkoani Arusha wametoa onyo kali kwa watu wenye tabia ya kuzusha, kuandaa, na kusambaza habari za uongo (Fake News) mtandaoni. Jeshi hilo limekumbusha kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kukiuka sheria za makosa ya mtandao kwa makusudi ili kuchafua amani ya nchi.