Upweke ni hali ya kukosa mtu unayemwamini wa kukusikiliza, mtu wa kukuelewa, mtu wa kukuamini, mtu unayemruhusu kujua upande wako wa pili na bado usiwe na wasiwasi. Upweke ni kukosa mtu unayekuamini, mtu anayeweza kukutetea na hata anapojua umeharibu anao ujasiri wa kukuonya na bado akaendelea kukuamini.
Unaweza kuzungukwa na kundi kubwa la watu na bado ukawa mpweke. Upweke si ukiwa. Kuna saa huwezi kukutana na ‘wewe’ bila kuwa peke yako. Upweke, tofauti na ukiwa, ni kilio cha nafsi inayojisikia kutengwa na mtu unayemhitaji. Upweke ni hisia za kupuuzwa, kutokusikika, kutokueleweka na kutokuaminika.
Tishio la kweli kweli na lenye madhara makubwa kwa utulivu na utimamu wa akili ya mwanadamu ni pale anapokosa imani na watu wanaomzunguka —kuhisi hahitajiki, hasikiki, hathaminiki, haeleweki na haaminiki. Nafsi ya mwanadamu huanza kuugua magonjwa mengi anapoanza kujisikia mpweke.